Saturday 31 May 2014

VIFO VYA WAJAWAZITO TANZANIA, SAWA NA AJALI TANO ZA NDEGE ZA ABIRIA KILA SIKU

Mkurugenzi wa mradi wa Evidence for Action Craig Ferla akizungumza na waandishi wa habari Tanzania wanaobobea kuandika habari za afya ya uzazi2012.

NA, GORDON KALULUNGA.

INATIA moyo kusoma makala hii ambayo inatoa mchango wake katika kuhamasisha jamii ya watanzania kufahamu ukubwa wa changamoto zinazowakabili mama zetu na vichanga wakati wa ujauzito na kujifungua.

Katika tukio hilo adhimu la kuleta uhai duniani inasikitisha mno kwamba akina mama na watoto wachanga wengi hufariki hapa nchini.

Ni muhimu pia kutolea ufafanuzi kuhusu baadhi ya taarifa zilizomo kwenye makala hii.

Shirika la Afya Duniani linakadiria kuwa wanawake 8,500 na watoto wachanga 50,000 hapa Tanzania hufariki kila mwaka katika kipindi cha ujauzito na kujifungua. Ni takwimu za kushtusha sana.

Ni muhimu kufafanua zaidi kuwa mtoto mchanga ni mwenye umri wa tangu siku 0 hadi 28, ikiwa ni pamoja na wanaozaliwa wameisha kufa.

Kuna idadi nyingine kubwa zaidi ya watoto walio chini ya miaka mitano ambao hufariki kila mwaka (kama ilivyojumuishwa kwa makosa kwenye makala hii, badala ya vichanga peke yake).

Ila izingatiwe kuwa vifo vya watoto katika siku 28 za kwanza za kuishi ni karibu theluthi moja ya vifo vyote vya watoto chini ya miaka mitano hapa Tanzania.

Ukichukua takwimu za wastani wa wanawake 8,500 na vichanga 50,000 wanaofariki wakati wa ujauzito na kujifungua kila mwaka nchini Tanzania, hii ni sawa na akina mama 23 na vichanga 137 wanaofariki kila siku.

Hili ni janga, hasa ukizingatia kuwa wengi wa akina mama na vichanga hawa wangeweza kuokolewa kama wangepata huduma bora.

Hata hivyo ni vigumu kuona na kuzingatia uhalisia wa kiwango na wingi wa vifo hivi katika maisha ya kila siku, hasa pale takwimu kubwa kama hizo zinapotumiwa.

Hivyo basi ndiyo sababu ukawekwa mfano huu kueleza ukubwa wa janga hili la kuwapoteza mama zetu na vichanga kila siku.


Ukisafiri ndani ya Tanzania kwa usafiri wa anga, kawaida ndege zinazotumika ni zile zenye kubeba abiria wapatao 30 hivi.

Na ndipo tulipoona muafaka kutumia mfano wa vifo vya akina mama 23 na vichanga 137 kila siku, kuwa ni kama ndege tano za abiria zingeanguka kila siku, ambapo kati ya hizo ndege tano, ndege moja ingebeba akinamama na nyingine nne zingebeba vitoto vichanga.

Kuielezea hali kwa namna hii ni kwa nia ya kufikisha ujumbe wa ukubwa wa janga hili linalozikumba familia na taifa kwa ujumla kila siku.

Hebu fikiria kama kungekuwepo kweli na ajali tano za ndege kila siku—kungekuwa na taharuki kubwa sana na wanajamii wa ngazi zote kulikemea jambo hili kudai likomeshwe mara moja, huku juhudi za kila aina zingefanywa lisitokee tena.

Ili kuboresha hali ya uzazi salama kwa kiwango kikubwa, ni muhimu sana wanawake wengi zaidi watafute nakupata huduma bora.

Iwapo kila mama atajifungulia kwenye kituo cha tiba ambacho kinatoa huduma bora, akina mama wengi na vichanga tunaowapoteza kwa sasa wataokolewa. Kwa sasa wanawake wanaojifungulia katika vituo vya afya bado ni wachache:

kwa mujibu wa utafiti wa Demografia na Afya Tanzania (TDHS) 2010 ni mwanamke mmoja tu katika kila wawili ndiye anayejifungulia katika kituo cha afya.

Yaani kigezo cha hatua hii muhimu ambayo ingeweza kuchukuliwa na kupunguza vifo vya mama na vichanga kwa kiasi kikubwa kimekuwa hivyo hivyo katika kipindi cha miaka 25 bila mabadiliko.

Hii ni tangu ulipofanyika utafiti wa TDHS wa kwanza 1990 ambapo ni nusu tu ya wanawake walikuwa wakijifungulia kwenye vituo vya afya.

Na japo kwa usahihi kabisa, makala hii imeeleza kuhusu ongezeko la idadi ya vizazi hai katika vituo vya afya, ieleweke kuwa pia ongezeko kubwa la idadi ya watu hapa Tanzania linamaanisha kuwa mfumo wa afya nao haujaweza kufanya mabadiliko ya kuendana na kiwango cha ongezeko la wanawake wanaojifungulia vituo vya afya kati ya mwaka 1986 na 2010.

Ujumbe mkuu hapa ni kuwa idadi kubwa ya akina mama na watoto wachanga wa Tanzania ambao maisha yao yanapotea wakati wa ujauzito na kujifungua kila mwaka yangeweza, na kwa hakika yanatakiwa kuokolewa.

Kila mtu, kwa nafasi yake katika jamii ni lazima atambue fursa zilizopo, zinazoweza kugeuza mwelekeo wa janga hili linalotokea kila siku.

Jitume, chukua hatua kuhakikisha mama zetu na vichanga wetu wanavuka salama kipindi hiki muhimu cha kuleta uhai.

No comments:

Post a Comment