Saturday 31 May 2014

FAIDA ZA WAJAWAZITO KUJIFUNGULIA VITUO VYA AFYA HIZI HAPA

IKIWA mkoa wa Mbeya una asilimia 57 ya wajawazito wanaojifungulia hospitali na vituo vya afya, wito umetolewa kwao kujitokeza kwa wingi kuhudhuria Kliniki ili kupunguza vifo vya mama na mtoto.

Wito huo umetolewa mwishoni mwa wiki na Mhadhiri, kaimu mkuu wa taasisi ya tiba ya St. Aggrey Jijini Mbeya, Dr. Karim Segumba.
 
Dr. Karim alisema kuwa faida wanazozipata wajawazito wanapohudhuria Kliniki ni pamoja na mjamzito kuchunguzwa afya yake kwa undani, ikiwemo umri wa mimba, kimo cha mimba, historia ya uzazi wa awali, uwingi wa damu, mkojo kwa protini na kutoa wasiwasi wa kifafa cha mimba.

‘’Mwanamke anachunguzwa shinikizo la damu, mlalo wa mtoto, mapigo ya moyo ya mtoto, ikibidi ultrasound kuangalia kama mtoto yupo hai, au ni mlemavu, ukubwa wa mtoto, kondo la nyuma la mama, kukomaa kwa mtoto, nyonga za mama kama zinaruhusu kujifungua kwa njia ya kawaida au upasuaji na anaelezwa tarehe ya makisio ya kujifungua’’ alisema Dr. Karim.
Mbali na uchunguzi huo, alisema kuwa mjamzito anayehudhuria kliniki anapimwa pia VVU na anapoonekana kuwa ana maambukizi anapewa mbinu za kumkinga mtoto aliye tumboni.

Alipoulizwa madhara yanayoweza kuwapata wajawazito ambao hawaendi kliniki na hawajifungulii hospitali na vituo vya afya, alisema ni pamoja na mjamzito kutoelewa maendeleo ya mimba yake na hatari ambazo zingeweza kugundulika na kutatuliwa na wataalam ili kuzuia kifo chake na mtoto.

‘’Hivyo ili kupunguza vifo vya mama na mtoto ni muhimu wajawazito wakahudhuria kliniki na kujifungulia katika vituo vya tiba na kizuri zaidi huduma zote hizo kwa mama mjamzito na mtoto chini ya miaka mitano hutolewa bure kote nchini’’ alisema mhadhili huyo.

Mratibu wa huduma ya mama na mtoto katika hospitali ya mkoa wa Mbeya Prisca Butuyuyu, alisema kwa sasa mkoa wa Mbeya, wajawazito wengi wanahudhuria kliniki lakini wengi wao wanajifunguli nyumbani.

Aliitaja wilaya ya Ileje kuwa ndiyo wilaya inayoongoza kwa wajawazito kujifungulia nyumbani, ambapo Jiji la Mbeya linaongoza kwa wajawazito wengi kujifungulia katika vituo vya tiba.

‘’Zaidi ya asilimia 40 wajawazito wanajifungulia nyumbani lakini baadhi wanajifungulia kwa wakunga wa jadi na njiani ingawa hatuna takwimu sahihi zaidi’’ alisema Butuyuyu.

Alisema Jiji la Mbeya wajawazito wanajifungulia hospitali hasa hospitali ya wazazi Meta kwa asilimia 109, Kyela 67, Chunya 58, Rungwe 55, Mbozi 45, Mbeya Vijijini asilimia 38 na wilaya ya Ileje asilimia 33.

No comments:

Post a Comment