WAKATI
imebakia miaka miwili kuhakikisha malengo ya milenia yanatekelezwa, baadhi ya
watoto wa kike nchini Tanzania, wamekuwa wakifukuzwa shule kutokana na
ujauzito, huku wengine wakiacha wenyewe masomo pale tu wanapojigundua ni
wajawazito.
Maeneo
ambayo ymebainika kuwepo kwa hatari hiyo inayoendelea kwa watoto hao wa kike ni
wilayani Ileje, Kyela mkoani Mbeya, Musoma mkoani Mara na Bagamoyo mkoani
Pwani.
Msichana Mwanaharusi
Mkupi (17) mkazi wa kijiji cha Yombo wilayani Bagamoyo mkoani Pwani, ambaye
anasema kuwa alikuwa na ndoto ya kuwa Daktari, ni mmoja kati ya wasichana waliokatisha masomo
yao kutokana na ujauzito alioupata akiwa darasa la tano.
Anasema alirubuniwa
na mvulana ambaye ni dereva wa pikipiki ,akajiingiza kwenye mahusiano ya
‘’ki-ngono’’ akapata ujauzito na kukatisha
masomo ya elimu ya msingi.
Mama yake
Mwanaharusi aliyejitambulisha kwa jina la Habiba Bakari (45) anasema, alijua
kama binti yake amepevuka lakini
hakuwahi kumfundisha masuala ya
afya ya uzazi kwani alikuwa akisubiri ahitimu darasa la saba ili amuweke ndani,
kwa ajili ya kumpa mafunzo ya namna ya
kujihadhari na wanaume, lakini akapatwa
na mshtuko baada ya kumuona mwanae ni mjamzito.
‘’Mila zetu mtoto wa kike anapopevuka hulazimika kukaa
ndani bila kuonekana na watu wengine ambao si wanafamilia, kwa muda wa mwezi
mmoja au zaidi, akifundishwa jinsi ya kujitunza na kujiepusha na vitendo vya
ngono’’ anasema Habiba.
Anasema
kutokana na utaratibu uliowekwa na
kijiji cha Yombo ni kwamba mtoto afanyiwe mafunzo hayo baada ya kumaliza darasa
la saba, basi hata yeye alikuwa akisubiri muda huo ufike, “nadhani kuna kitu
nilitakiwa kufanya lakini kwa sasa nimechelewa” anasikikitika.
Wakati mama
yake Mwanaharusi akijilaumu kwa
kushindwa kumfundisha mwanae namna ya kujikinga na ujauzito, Pili Amada (17) naye amejikuta akipata ujauzito akiwa na
umri wa miaka 16, hali ambayo anaijutia kwani hana biashara yoyote
inayomwingizia kipato na kujikuta akimtegemea mama yake kwa malezi ya mwanae.
Anasema
alipata ujauzito akiwa tayari amepata mafunzo ya kimila, lakini anaweka wazi
kwamba alipokuwa ndani alikokuwa akifundishwa, aliambiwa kwamba ameshapevuka hivyo akikutana na mwanaume
atapata ujauzito.
Anatanabaisha kuwa licha ya kuambiwa hivyo, hakuwahi
kuambiwa kuhusu namna ya kujikinga ndipo akajiingiza kwenye vitendo vya ngono na kupata ujauzito.
Anasema
anajisikia vibaya kumuona mama yake
ambaye ni mkulima, akihangaika kutafuta mahitaji yake pamoja na mwanae kazi
ambayo angetakiwa kuifanya yeye na mwenza wake aliyempa ujauzito.
Anasema hana
namna nyingine ya kufanya kwani tangu mwanaume alipompa ujauzito hajawahi
kupeleka matunzo ya mtoto.
Pili ambaye
alipata ujauzito baada tu ya kumaliza darasa la saba, anasema akiwa shuleni
hakuwahi kufundishwa njia za kujikinga
na ujauzito, zaidi ya kuambiwa
mabadiliko ambayo atayapata atakapopevuka lakini hiyo haikuwa kinga ya kushinda
vishawishi vya wanaume.
Mganga mkuu
wa zahanati ya Yombo, Donald Malamsha anasema wasichana wa kijiji hicho hasa
wanafunzi wa shule ya msingi, wanaogopa kufika zahanati kupata ushauri wa namna ya kujikinga na
ujauzito kwa kile alichokiita “kuona aibu” kwamba wataonekana wanajihusisha na vitendo vya ngono wakiwa
bado wadogo.
‘’Wasichana
wengi hufika katika hapa kupata ushauri
wa kutumia njia za uzazi wa mpango, wakiwa tayari na watoto’’ anasema Mganga
huyo.
Malamsha,
anasema athari zinazoweza kujitokeza kwa wasichana ambao hawajafikisha umri wa
miaka 18 wanapopata ujauzito, anasema mara nyingi huvuja damu nyingi wakati wa
kujifungua.
Anasema upo
uwezekano mkubwa wa kuzaa mtoto ambaye hajafikisha miezi tisa tumboni (njiti),
pia mtoto atakayezaliwa, anaweza kupata utindio wa ubongo na msichana kupata
uzazi pingamizi na hatimaye kufanyiwa upasuaji wakati wa kujifungua.
Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Yombo, Ostina Gama
anakiri kwamba katika shule yake wanafunzi wengi wa kike wanakatisha masomo kutokana na kupata mimba.
Anasema
wakati somo la sayansi lenye mada za
uzazi likifundishwa darasa la saba na darasa la sita, baadhi ya wanafunzi hupata ujauzito wakiwa darasa la nne na darasa
la tano kabla hawajapata elimu hiyo.
Diwani wa
kata ya Yombo, Idd Mazongela, anakiri kuwepo kwa tatizo la mimba za utotoni
katika kata yake, anasema kwa sasa anaomba mashirika na taasisi binafsi
zinazotoa elimu ya afya ya uzazi shuleni, kutembelea kata yake kwani anaamini
elimu ya afya ya uzazi ikifundishwa kikamilifu basi tatizo la mimba za utotoni
litaondoka.
Anasema
wanafunzi wanaopata ujauzito mara nyingi hurubuniwa na vijana wenzao, hali
inayoonyesha kukosekana kwa elimu ya afya ya uzazi kwa jinsia zote yaani vijana
wa kike na wa kiume.
Afisa elimu
wa wilaya ya Bagamoyo, Juma Kabelwa, anasema kwa sasa tatizo la mimba za
utotoni limepungua kidogo katika wilaya hiyo ikilinganishwa na miaka ya nyuma.
Anasema kwa
mwaka jana 2012, ni mwanafunzi mmoja tu kwa wale waliojiandikisha kufanya
mtihani wa darasa la saba katika wilaya
nzima ambaye alikutwa na ujauzito.
Takwimu za
wizara ya elimu na mafunzo ya ufundi za mwaka 2010, zinaonyesha kuwa wanafunzi 500 walikatisha
masomo katika mkoa wa Pwani pekee, kati
ya mwaka 2005 na 2009 kutokana na ujauzito.
Kwa upande
wa wilaya ya Kyela mkoani Mbeya, nako hali hiyo ya watoto wa kike kupata
ujauzito wakiwa bado hawajafikisha umri wa miaka 18, unaotambulika kikatiba kuwa mtu mzima.
Josephine
Boazi (17) mkazi wa kijiji cha masoko kata ya Busale wilayani Kyela, alikatisha
masomo yake akiwa kidato cha kwanza kutokana na kupata ujauzito.
Anasema
hakuwahi kufundishwa namna ya kujikinga na ujauzito, kwa sasa yupo nyumbani
akiwategemea wazazi wake katika kumlea mwanae na yeye pia.
Mama yake
Josephina, aliyejitambulisha kwa jina la Stella Mbukwa, anasema si jambo la
kawaida kwa mama kuzungumzia masuala ya uzazi kwa binti yake kwani ni kitu
ambacho hakipo katika mila na desturi zao.
Wakati
Stella akiona aibu kuzungumza na binti yake, tamko la serikali kuhusu
uzazi wa mpango kwa vijana , linasema
vijana wote wana haki ya kupata taarifa, elimu na ushauri nasaha kuhusu
njia za uzazi wa mpango, tamko ambalo Stella anakiri kuwa hajawahi kuliona wala
kulisikia.
Katika
wilaya ya Ileje mkoani Mbeya, nako kuna idadi kubwa ya wanafunzi wanaoacha
masomo kutokana na mimba za utoto ambazo baadhi zinaambatana na maambukizi ya
virusi vya Ukimwi(VVU).
Mkurugenzi
wa shirika lisilokuwa la kiserikali la Hossana Ows Centre la wilayani humo
linaloshughulika na masuala ya afya, Nsanya Mwalyego, anasema kuwa mpaka sasa
shirika lake linahudumia zaidi ya wananchi 350 ambao wanaishi na maambukizi ya
virusi vya ukimwi.
Anasema
idadi hiyo ni ya wananchi waliopo katika kata nne tu kati ya kata kumi na nane
zilizopo katika wilaya hiyo ya ileje.
‘’Tuanahudumia
watu 350 waliojitokeza katika kata nne ambazo ni Itumba, Isongole, Chitete na
Mlale tu ambao tunawafundisha jinsi ya kujikinga na maambukizi mapya,
kutojinyanyapaa na tunawapatia dawa baridi kwa wagonjwa wa majumbani wakiwemo
wenye vidonda’’ alisema Mwalyego.
Kaimu
mratibu wa kitengo cha Ukimwi mkoa wa Mbeya Dr.Francis Philly, anasema kuwa
mwitikio wa wagonjwa wanaotumia dawa za ARV kuwa ni mkubwa kwani takwimu
zinaonesha kuwa kuanzia June 2004 hadi June 2012 wagonjwa waliojiandikisha
katika huduma ni 106598 ambapo watu wazima ni 92085 na watoto ni 12889.
Kwa mujibu
wa sera ya taifa ya afya ya uzazi ya mwaka 2007, inasema uzazi wa mpango ni
haki ya kimsingi ya kila mtu, bila kujali kama ameolewa au kuoa na kama amezaa
au hajazaa.
Wakati sera
ikisisitiza kuwa uzazi wa mpango ni haki ya kila mtu, Pili Makuri (18) mkazi wa
kijiji cha Bweri, wilaya ya Musoma mkoani Mara, anasema alipata ujauzito akiwa
darasa la tano na akiwa na umri wa miaka 16 alizaa kwa upasuaji, kutokana na
nyonga yake kuwa ndogo, kulingana na umri wake
mdogo.
Lakini mtoto
akiwa na mwaka mmoja akapata ujauzito mwingine ambao ulimfanya afanyiwe tena
upasuaji,. anakiri kwamba hali hiyo
imetokana na kutokufahamu njia za kuzuia
ujauzito usiotarajiwa.
Ripoti ya
wizara ya afya na ustawi wa jamii ya mwaka 2011 inaonyesha kwamba, asilimia 25 ya wanawake walio katika
umri wa kuzaa ambao wangependa kupumzika, kupangilia uzazi, hawatumii njia yoyote za uzazi wa mpango.
Utafiti wa Shirika
la afya Duniani (WHO) na (UNFPA), kuhusu masuala ya mimba za utotoni, unaonyesha kuwa
wasichana milioni 14 mpaka 15 ambao wako chini ya umri wa miaka 18 wanakuwa tayari wana watoto kwa kila mwaka, hii ikionyesha kuwa ni sawa
na asilimia 10 ya uzazi
kwa dunia nzima.
Malengo ya
Milenia yaliyotamkwa na nchi 193
wanachama wa Umoja wa Mataifa (UN) mwaka 2005 mjini New York Marekani, yamelega
kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2015,
watoto wote wa kiume na wa kike
waweze kumaliza masomo yao ya
elimu ya msingi.
Uchunguzi
uliofanywa na mwandishi wa makala haya mkoani Mbeya, Pwani na mkoani Mara
katika wilaya za Ileje, Kyela, Bagamoyo, Bunda, Butiama na Musoma, umebaini
kuwa watu wengi wanaotumia mipira ya kiume (Kondomu), huwa wanatumia siku ya
kwanza mpaka ya tatu na baada ya hapo hawatumii kabisa na baadhi wanapokutana
na wanafunzi wa kike huwa hawatumii hata siku ya kwanza.
No comments:
Post a Comment